Thursday, February 7, 2013

NAMNA YA KUJIPANDISHA THAMANI KWA MPENZI WAKO!

KAMA si Mungu, maisha yangu si lolote. Sina ujanja wa kufanya chochote bila msaada wake, hii ndiyo sababu inayonifanya siku zote nimuinue na kumtukuza kwa nguvu kwa maana yeye ndiye mwongozo wangu.
Karibuni marafiki zangu katika uwanja wetu ambao hupanua mawazo yetu ndani ya ulimwengu wa mapenzi. Leo nahitaji kuzungumza nanyi jambo moja muhimu sana; kujipandisha thamani kwa mpenzi wako.
Kuna wakati inatokea kwenye uhusiano, mmoja wao (hasa mwanamke) akadhauriwa na mpenzi wake na kuonekana wa kawaida tu. Athari kubwa zaidi katika kuonekana wa kawaida au kudharauliwa ni kuachana wakati wowote – kwa ghafla.
Mara nyingi tendo la kuachana kwa wenzi wa aina hii huwa hakuna sababu kubwa sana. Jambo dogo tu, linaweza kukatisha uhusiano, lakini kumbe ndani kuna siri nyingine kubwa zaidi; kushuka thamani kwa mpenzi wako.
Marafiki zangu, wakati uhusiano unapofikia kwenye hatua hii huwa ni hatari sana na uamuzi wa kuachana hupewa nafasi kubwa sana tena kwa pande zote. Habari mbaya zaidi ni kwamba, hata kama wahusika watakuwa wana ndoa, huwa si kigezo kikubwa sana kwao, badala yake hufikiria kuachana kama ndiyo kitulizo cha mioyo yao.
HEBU TUJIFUNZE
Nazungumzia kuhusu thamani. Ni somo linalohitaji utulivu mkubwa wa akili na utayari wa ubongo. Ninaposema kushuka thamani namaanisha kupungua kwa umuhimu au kupotea kabisa.
Kubwa ambalo utakuwa umebaki nalo (labda) ni kukutana kwa ajili ya mapenzi tu. Hawezi kukushirikisha katika mambo yake kwa sababu huna thamani kwake.
Kwa bahati mbaya ni kwamba, ukishushwa thamani, mara nyingi unaweza usigundue hilo hivyo kuendelea na maisha kama kawaida katika mtindo ambao kumbe tayari mwenzako ameshakubadilisha daraja.
UTAJUAJE KUWA UMESHUSHWA THAMANI?
Ninachohitaji kuzungumza nanyi marafiki zangu ni namna ya kujipandisha thamani ili mpenzi wako asikuchoke wala kukushusha au kukuona wa kawaida. Kila wakati akione wewe ni muhimu na akufanye namba moja katika maisha yake lakini kabla sijafika hapo nataka kwanza mfahamu dalili atakazozionyesha mwenzako kuonesha kwamba ameshakushusha thamani.
(i)  Mawasiliano hupungua
Hapa inategemea na kasi ya mawasiliano mliyokuwa nayo mwanzoni lakini kwa kiwango chochote kile huanza kupungua. Kama alikuwa na kawaida ya kuwasiliana nawe mara kwa mara akikueleza mambo mbalimbali – hata madogo tu, kuhusu mwenendo wa siku yake, ataacha.
(ii) Msiri kupitiliza
Kulingana na kiwango cha uhusiano wenu, ataanza kuwa msiri kwa baadhi ya mambo yake. Hata kama anafanya jambo fulani zuri kwa ajili ya maisha yenu ya baadaye, hatakuambia. Unaweza kushtukia tu kusikia kwa watu kuwa mwenzako ameagiza gari au amenunua kiwanja mahali  na pengine ameshaanza ujenzi bila kukujulisha.
(iii) Hukupuuza
Kama awali alikuwa na kawaida ya kukusikiliza, sasa ataanza kukupuuza. Unaweza kumwambia jambo lenye manufaa makubwa sana kwenu lakini asilichukulie umakini. Hii ni dalili kwamba wewe huna thamani kwake.
(iv) Hataki maswali
Mara nyingi mtu wa aina hii huwa na tabia ya kutokutaka kujadiliana kwa hoja. Kwa mfano hataki kuulizwa alipokuwa na ratiba zake zijazo. Huanza kuwa na jazba na hataki kabisa maswali yoyote kuhusu utaratibu wa maisha yake.
Ukiona alama hii ujue kuwa tayari mwenzako ameshakushusha thamani.  Marafiki, natamani kuendelea zaidi lakini nafasi yangu ni ndogo. Kwa leo naomba kuweka kituo kikubwa hapa, wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayendikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments:

Post a Comment